Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Khalfan Haule leo ameongoza kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe katika Mkoa wa Mara kwa Mwaka 2023/2024 na kupongeza kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utekelezaji wa mkataba wa lishe.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi, Mhe. Haule amesema katika afua nyingi za lishe Mkoa wa Mara umepiga hatua kubwa ikiwemo ya utengaji wa fedha za utekelezaji wa mkataba wa lishe.
“Wakati tunaanza kutekeleza mwaka 2017/2018 Mkoa wa Mara ulikuwa unatumia chini ya asilimia 18 ya fedha zilizotengwa, lakini kwa mwaka huu uliopita Mkoa wa Mara umetumia kwa zaidi ya asilimia 95 ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Mkataba wa lishe” amesema Mhe. Haule.
Mhe. Haule amezitaka Halmashauri kuongeza fedha inazotenga kwa ajili ya masuala ya lishe ili kuongeza utoaji wa huduma za lishe kwa walengwa na kupunguza changamoto ya utapiamlo na kuzitaka kutenga zaidi ya shilingi 1000 kwa kila mtoto.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Musoma amezielekeza Halmashauri zilizopo mjini kama vile Mji wa Tarime, Manispaa ya Musoma na Halmashauri ya Mji wa Bunda ziongeze fedha zinazotengwa kutokana na kuhudumia watu wengi zaidi kuliko Halmashauri za Wilaya.
Mhe. Haule amewataka Wakurugenzi kuhakikisha Vitengo vya manunuzi vinaingiza kwenye mfumo wa manunuzi manunuzi yote yanayofanyika ili Halmashauri ziweze kupata taarifa sahihi za manunuzi kwenye mfumo kulingana na manunuzi yaliyofanyika na hususan katika afua za lishe.
Akitoa taarifa ya tathmini Kaimu Afisa Lishe Mkoa wa Mara Bi. Grace Martin Mgongolwa amesema katika kipindi hicho, matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya lishe katika bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ni shilingi 758,966,854.86 ambapo kati yake shilingi 724, 545,126.77 zimetumika.
“Hii ni sawa na asilimia 95.5 ya fedha zote zilizopangwa kutumika kutekeleza afua za lishe katika Mkoa wa Mara ambapo hata hivyo baadhi ya fedha iliyotumika haikujazwa kwenye mfumo wa manunuzi na wataalamu wa manunuzi na hivyo kupunguza asilimia ya fedha zilizotumika” amesema Bi. Mgongolwa.
Bibi Mgongolwa ameyataja maneo ambayo bado yanachangamoto kuwa ni idadi ndogo ya wanafunzi wanaokula chakula shuleni, ukosefu wa mizani wa kupima uzito vijijini, ukosefu wa virutubishi vya kutimu watoto wenye utapiamlo wa kadri na upungufu wa chakula dawa cha kutibu watoto wenye utapiamlo mkali.
Bibi Mgongolwa amezitaka Halmashauri kuweka sheria ndogo zitakazohakikisha shule zote zinatoa chakula shuleni, kutenga fedha kwa ajili ya kununua vibao na mizani wa kupima uzito katika vituo vya kutolea huduma za afya, kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa chakula chenye virutubishi kwa ajili ya watoto wenye utapiamlo mkali na kuimarisha upatikanaji wa takwimu za udumavu.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Menejimenti ya Mkoa wa Mara, Meya na Wenyeviti wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, baadhi ya wakuu wa Idara za Halmashauri na Timu ya uendeshaji wa shughuli za afya Mkoa wa Mara (RHMT).
Butiama District Council
Anuani ya posta: P.O.BOX 1207 BUTIAMA
Simu: (028)2623121
Simu: 0767300061/756357458
Barua pepe: ded@butiamadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Butiama.Haki zote zimehifadhiwa